ELCT Press Release

Date: June 30, 2017
Press release No. 002/06/2017

close window


Mkutano Mkuu wa 24 wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati wamalizika kwa amani
Na Elizabeth Lobulu

Mkutano Mkuu wa 24 wa Dayosisi ya Kaskazini Kati ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) umemalizika kwa amani na wajumbe wake wameahidi kuendeleza mshikamano na umoja katika Dayosisi na Kanisa kwa ujumla.


Askofu Dkt. Solomon Massangwa, alipokuwa akifungua
Mkutano 28 Juni 2017.

Mkutano Mkuu wa Dayosisi ulifanyika miaka mitatu iliyopita ambapo Askofu Dkt. Solomon Massangwa alichaguliwa kuwa Askofu kuchukua nafasi iliyoachwa wazi baada ya Askofu Dkt. Thomas Laiser kuitwa mbinguni.

Akifungua mkutano huo uliofanyika Shule ya Sekondari Peace House, Arusha, mnamo 28 Juni 2017, Askofu Dkt. Massangwa aliwataka watu wote wakiwemo wanadayosisi, kuendelea “kumtazama Mwana kondoo wa Mungu” aondoaye mizigo na mahangaiko yote mtu aliyonayo.


“Japo kidunia watu huwaambia watoto wao watawapa urithi wa elimu, magari au nyumba lakini mwishowe vitu hivi vyote tutaviacha. Ila urithi ulio mzuri ni kumtazama zaidi Yesu kwa kumwamini la sivyo tutabaki na mizigo yetu,” alisema.Baadhi ya viongozi waliokuwepo siku ya ufunguni kuanzia kushoto: Askofu Charles Mjema,
Askofu Chediel Sendoro wakifuatiwa na wenyeji wao: Askofu Dkt. Solomon Massangwa,
Msaidizi wa Askofu, Mchg. Gideon Kivuyo na Katibu Mkuu, Bibi Rose Samwel Makara.

Mkutano Mkuu huo uliofanyika 27 - 29 Juni 2017 uliongozwa na kauli mbiu: “Mungu kwetu ni kimbilio na nguvu, msaada unaoonekana tele wakati wa mateso,” (Zab. 46: 1) ambapo mfundishaji wa Somo la Biblia alikuwa ni Askofu Chediel Sendoro wa KKKT Dayosisi ya Mwanga.


Baadhi ya wajumbe wa Mkutano uliofanyika Shule ya Sekondari Peace House, Arusha.

Askofu alitoa shukrani za dhati kwa wanadayosisi kwa kujitoa kulipa deni la benki lililokuwa linaikabili Hoteli ya Dayosisi, Corridor Springs, na kusema deni hilo limepungua kwa kiasi kikubwa kudhihirisha kwamba “Mungu kwetu ni kimbilio na nguvu”. Pia alihimiza waendelee kuchangia sehemu iliyobaki.


Mkuu wa KKKT, Askofu Dkt. Fredrick Shoo (kushoto),
aliusalimu Mkutano tarehe 29 Juni 2017.

Askofu alimtambulisha Bibi Rose Samwel Makara kuwa ni Katibu Mkuu mpya wa Dayosisi aliyechukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Samwel Njake ole Saiguran aliyeitwa mbinguni.

Akitoa salamu zake Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Pare Askofu Charles Mjema aliwapongeza wanadayosisi kwa kazi nzuri wanazofanya na kusema “iwapo Mungu ametenda kwa kanisa kwa kuwaondoa kwa kiasi kikubwa katika changamoto ya madeni; anaweza kukuokoa maana Mungu akiwa upande wako kila kitu ni salama.”

(Habari na Picha na Elizabeth Lobulu)

==================================================
Elizabeth Lobulu
Communication Coordinator,
Evangelical Lutheran Church in Tanzania
Box 3033, ARUSHA, Tanzania.
Phone: +255-27-250-8856/7
FAX: +255-27-254-8858
E-mail: ELobulu@elct.or.tz

Close this window

For more information contact:

Elizabeth Lobulu
Communication Desk Officer, ELCT
E-mail: ELobulu@elct.or.tz