ELCT Press Release

Date: May 16, 2017
Press release No. 001/05/2017

close window


Askofu Mkuu Musa Filibus awa Rais wa FMKD
Na Elizabeth Lobulu --- Windhoek, Namibia

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kikristo la Nigeria (LCCN), Dkt. Musa Panti Filibus, amekuwa Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (FMKD) alipoingizwa kazini katika ibada ya kufunga Mkutano Mkuu wa 12 wa jumuiya hiyo uliofanyika Windhoek, Namibia tarehe 10 - 17 Mei 2017.

Mkutano huo uliohudhuriwa na watu 800 ulikuwa na kauli mbiu: “Tumeokolewa kwa neema ya Mungu”. Na wajumbe walipata nafasi ya kusikiliza na kujadili mada ndogo tatu: “Wokovu si wa kuuzwa”; “Binadamu si wa kuuzwa” na “Uumbaji si wa kuuzwa”.


Rais mpya wa FMwa KD Askofu Mkuu Dkt. Filibus Musa akiwa na Askofu Younan Munib anayeondoka.

Mkutano huo ulikuwa wa kipekee kwa kuwa pamoja na mambo mengine ulikuwa na sherehe ya kukumbuka miaka 500 ya matengenezo ya kanisa kimataifa wakati wa Ibada ya Meza ya Bwana iliyofanyika Uwanja wa Taifa wa Sam Nujoma Windhoek tarehe 14 Mei 2017.

Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu: ‘Tunaokolewa kwa Neema ya Mungu’, pamoja na mambo mengine, ulipokea na kujadili hotuba ya Rais anayeondoka Dkt. Younan; Ripoti ya Katibu Mkuu wa Fungamano, Mch. Dkt. Martin Junge; mada mbalimbali na kufanya uchaguzi wa Rais na wajumbe wa Halmashauri Kuu.

Japo alianzia ngazi ya chini eneo la Mayo-Belwa, Askofu Mkuu Musa Panti Filibus, alichukua mafunzo ya ualimu daraja la pili na hatimaye kufundisha katika shule za serikali eneo la Mayo-Belwa.

Askofu Mkuu Filibus baadaye alijiunga na Chuo cha Theolojia Kaskazini mwa Nigeria (TCNN) na kufuzu Shahada ya Mafunzo ya Dini (Bachelors of Divinity Degree) mwaka 1992. Aliajiriwa kufundisha katika Seminari ya Ndogo ya Kilutheri Bronnum iliyoko Mbamba Yola, Jimbo la Adamawa kuanzia 1993.

Dkt. Musa alibarikiwa kuwa mchungaji mwaka 1994 kisha akaenda Marekani kusoma katika Chuo Kikuu cha Kilutheri Minnesota na kupata Shahada ya Udakatari katika masuala Theolojia na Unasihi Kichungaji.

Alipomaliza mashomo yake alirudi kufundisha katika shule alikotoka ambapo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo hicho hadi mwaka 2002 alipopokea wito kufanya kazi FMKD kama Katibu wa Afrika katika Idara ya Misioni na Maendeo Oktoba 2010. Aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara hiyo 2010 hadi Julai 2013.

Askofu Mkuu Musa Panti Filibus aliteuliwa na Kanisa lake kuongoza Dayosisi ya Mayo Belwa iliyoko kusini Magharibi mwa Nigeria na aliwekwa wakfu na kuingizwa kazini Oktoba 2013. Alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makanisa ya Kilutheri Nigeria ndipo Novemba mwaka jana akachaguliwa kuwaAskofu Mkuu LCCN.

Februari 2017 Makanisa toka Bara la Afrika yalimteua Askofu Mkuu Filibus kuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Fungamano.

Askofu Musa anachukua nafasi ya Askofu Dkt. Munib Younan wa Kanisa la Jordan na Nchi Takatifu aliyemaliza kipindi chake 17 Mei 2017.

==================================================
Elizabeth Lobulu
Communication Coordinator,
Evangelical Lutheran Church in Tanzania
Box 3033, ARUSHA, Tanzania.
Phone: +255-27-250-8856/7
FAX: +255-27-254-8858
E-mail: ELobulu@elct.or.tz

Close this window

For more information contact:

Elizabeth Lobulu
Communication Desk Officer, ELCT
E-mail: ELobulu@elct.or.tz