ELCT Press Release
Tarehe: 13 Juni 2013
Press release No. 001/06/2013

Click here for English

Funga "window" hii

KKKT kuadhimisha miaka 50

Wageni wapatao 5,000 wanatarajiwa kuhudhuria matukio ya kilele cha jubilii ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) tarehe 22 na 23 Juni 2013 kukumbuka miaka 50 tangu makanisa saba ya Kilutheri nchini kuungana na kuunda kanisa moja.

Katibu Mkuu wa KKKT, Bw. Brighton Killewa alisema hivi karibuni, kilele kitaadhimishwa katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Tumaini University Makumira -TUMA), Usa River kinachomilikiwa na KKKT kitakuwa na matukio ya siku mbili.


Ndg. Brighton Killewa, Katibu Mkuu KKKT

Alisema Juni 22 litakuwepo kongamano ambapo mada tano zitajadiliwa kuhusu kazi za Kanisa miaka 50 iliyopita na nini kifanyike kwa miaka 50 ijayo. Siku ya Jumapili 23 Juni ndipo itafanyika Ibada.

Kanisa linatarajia wageni wapatao 5,000 toka ndani na nje ya nchi kuhudhuria maadhimisho hayo yatakayofanyika Usa River, nje kidogo ya jiji la Arusha. Wageni wa nje ni kutoka makanisa na vyama vya misioni vya Afrika, Ulaya na Marekani. Kutoka ndani ni pamoja na wawakilishi wa Dayosisi za KKKT, viongozi wa Serikali na wa dini na kwaya.

Chuo cha Makumira ni mojawapo ya vituo vya pamoja kama Kanisa (vijulikanavyo kama vituo vya Kazi za Umoja KKKT) kinachounganisha dayosisi zote 22 za KKKT. Ni kituo cha mafunzo kilichoanza kama chuo cha Theologia hivyo viongozi wa kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki, Kati, Kusini na Magharibi mwa Afika na Mashariki ya Mbali wakiwemo Wachungaji na Maaskofu wamesoma katika chuo hicho. Chini ya mpango wa kubadilishana wanafunzi baadhi ya wanafunzi na wakufunzi wametoka Ulaya na Marekani.

KKKT ni muungano wa makanisa saba ambayo baadhi yao yalianza kutekeleza utume wa Mungu wa kueneza Injili nchini zaidi ya miaka 150. Tarehe 19 Juni 1963 viongozi wa makanisa hayo saba kwa hiari yao waliweka tofauti zao kando na kuamua kuunda Kanisa moja na kugeuza makanisa yao kuwa sinodi au dayosisi za KKKT.

Kadiri muda ulivyokwenda KKKT ikakubaliana kuacha mfumo wa sinodi na kuwa na mfumo wa Dayosisi. Hadi 26 Mei 2013 Dayosisi za KKKT zimefikia 22 baada ya mbili kuzinduliwa mwaka huu wa Jubilii. Nazo ni Dayosisi ya Kusini Mashariki (Mtwara/ Lindi) iliyozinduliwa Jumapili 26 Mei 2013 na Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria (Shinyanga/ Simiyu) iliyozinduliwa 5 Mei 2013.

==================================================
Elizabeth Lobulu
Communication Coordinator,
Evangelical Lutheran Church in Tanzania
Box 3033, ARUSHA, Tanzania.
Phone: +255-27-250-8856/7
FAX: +255-27-254-8858
E-mail: Elizabeth Lobulu <ELobulu@elct.or.tz>

Funga "window" hii

For more information contact:

Elizabeth Lobulu
Communication Desk Officer, ELCT
E-mail: ELobulu@elct.or.tz