ELCT Press Release
Date: Septemba 3, 2010
Press release No. 001/09/2010

Washiriki 2000 wa wahudhuria mkutano Dodoma

Washiriki wapatao 2000 walihudhuria mkutano wa wachungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) uliofanyika Dodoma 28 Agosti hadi 1 Septemba mwaka huu.

Lengo kuu la Mkutano huo ambao ulikuwa na Neno Kuu kutoka 2 Kor 5: 20: "Ushuhuda wetu," lilikuwa kutafakari kwa pamoja kuhusu nafasi waliyonayo Wachungaji katika huduma wanayotoa. Askofu Mstaafu Elinaza Sendoro ndiye aliyeongoza Somo la Biblia.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mkuu wa KKKT Askofu Dkt Alex Gehaz Malasusa aliwataka Wachungaji hata kama watalaumiwa kwa kukaripia au kuonya maovu wenyewe wasiwe watu wa "kulaumika".

Mkuu wa KKKT alisema "ushuhuda" ni jukumu ambalo shahidi anabebeshwa ili aufikishe mahali unapotakiwa ukae na kwamba Wachungaji ni mashahidi wa Kristo waliopewa "ushuhuda" ambao ni Injili ya Kristo inayookoa ili kuipeleka hadi mwisho wa nchi (Mdo 1:8). Pia alisisitiza mafundisho ya Mtume Paulo anaposema, "Sisi tu mashahidi na mawakili wa siri za Mungu".

Wajumbe walipata nafasi ya kusikia na kujadili mada kama vile "Umoja wa Wachungaji" iliyoongozwa na Mkuu Mstaafu wa KKKT Askofu Dkt. Samson Mushemba; "KKKT na Makanisa Mengine" ambayo ilikuwa na sehemu iliyoongozwa na Askofu Dkt. Israel-Peter Mwakyolile (Dayosisi ya Konde) na sehemu ya pili ilitolewa na Mchg. Dkt. B. Holmberg kutoka Sweden.

Mada nyingine zilihusu "Vimbunga vya Mafundisho Potofu" (Askofu Dkt. O.M. Mdegella, Dayosisi ya Iringa); "Roho ya Ibada katika KKKT" (Mchg. Dk. E. Mungure, Chuo Kikuu Kishiriki Makumira); "Urithi Wetu" (Mchg. Dkt. W. Niwagila, Dayosisi ya Kaskazini Magharibi); "Wajibu wa Kichungaji katika Kufundisha na Kuhubiri" (Ask. Dkt. H. Mwakabana, KKKT Dayosisi ya Kusini Kati).

Mada nyingine ilikuwa: "Jukumu la Kanisa katika Utetezi" iliyotolewa na Askofu Dkt. Stephen Munga (KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mashariki) ambapo alieleza adha ya wakazi wa Tarime Mkoani Mara walipotumia maji ya mto Tigite na kuathirika kwa kemikali zinazotokana na uchimbaji mkubwa wa dhahabu ambao haukuwa unazingatia utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

Wajumbe waliona sinema iliyotengenezwa 2009 baada ya utafiti uliofanywa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa ushirikiano na NCA (Norwegian Church Aid) ilionyesha jinsi maji, viumbe hai kama samaki vimetoweka na binadamu walivyoathirika ngozi na watoto kuugua tumbo.

Katika mkutano huo wa siku tano uliofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma, wajumbe pia walijadili na kuridhia "Tamko la Dodoma" ambalo linafafanua kwa nini KKKT inapinga ndoa za jinsia moja. Tamko la Dodoma ambalo linapatikana katika tovuti ya KKKT: "www.elct.org" lilipitishwa na Halmashauri Kuu ya KKKT mwanzoni mwa mwaka 2010.

Mkutano wa Wachungaji kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 1997 katika Chuo cha Ualimu Kigurunyembe mjini Morogoro.

Imetolewa na:
Ofisi ya Katibu Mkuu KKKT.

==================================================
Elizabeth Lobulu
Communication Coordinator,
Evangelical Lutheran Church in Tanzania
Box 3033, ARUSHA, Tanzania.
Phone: +255-27-250-8856/7
FAX: +255-27-254-8858
E-mail: Elizabeth Lobulu <ELobulu@elct.or.tz>

Close this window

For more information contact:

Elizabeth Lobulu
Communication Desk Officer, ELCT
E-mail: ELobulu@elct.or.tz